Kala Tufaha By OMAR

by sava in Text book centre buy now Publishered by: sava

Kala Tufaha By OMAR Details


Hii ni riwaya ninayoiashiki mno. Imeandikwa na Omar Babu Marjan (Abu Marjan), msomi, mwandishi na mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Cologne nchini Ujerumani. Japo nimevisoma vitabu vingi, Kala Tufaha ni baadhi ya riwaya zilizoandikwa zikaandikika. Kala Tufaha ni hadithi inayoyaelezea maovu wanayofanyiwa wanawake; kutosomeshwa, kubakwa na kupuuzwa. Inaelezea kuhusu msichana anayeitwa Kibibi (Tufaha). Japo alikuwa mwerevu darasani, ndoto yake ya kujiunga na shule ya upili inakatizwa wakati baba yake anakataa aendelee na masomo ili aolewe. Ingawa alikuwa wa kwanza Tarafani na wa pili Wilayani katika mtihani wa shule za misingi, alibaki kuajiriwa katika mtaa wa mabwanyenye. Mara, tajiri wake, Fumbwe, anammezea mate na kumbaka, jambo ambalo Kibibi hakusaidika katika kituo cha polisi kwa kuwa aliyembaka alikuwa Mkuu wa Idara ya Ujasusi. Kesi ilifutiliwa mbali hata amjaribu wakili. Kibibi, mwenye bidii, anaizumbua riziki angaa ajikimu na kumkuza mwanawe, Kala, ambaye mwishowe anakuwa daktari. Dakta Kala Tufaha anamfanyia fadhili Fumbwe hospitalini katika uzee wake. Dakika ya mwisho, Fumbwe anaaga na papo hapo Dakta Kala Tufaha kugundua kuwa, Fumbwe, alikuwa baba yake mzazi, jambo ambalo hakulijua zaidi ya mwaka mzima alipokuwa akimhudumia huyo mgonjwa wake. Riwaya yenyewe inao mtiririko na lugha iliyoandikwa kwa ustadi mno. Fauka na hayo, inaelezea kuhusu matukio yanayofanyika kila uchao katika jamii ya kisasa; serikalini, barabarani, mitaani, nyumbani nk. Aidha, matumizi ya taharuki yanamwabirisha msomaji chombo cha tamaa ya kuendelea kusoma ambapo mara kwa mara analiwazwa mtima na mbinu-rejeshi. Ucheshi na vichekesho si haba, kando na kumsairi msomaji kuwa mcha Mungu na dhabiti kwa imani ya kidini. Aliyekisoma kitabu hiki, bila shaka, atakueleza uzuri wake.

ISBN: 9966472851 SKU: 2010143000430