Kiti cha Moyoni na hadithi nyingine ni mkusanyiko wa hadithi fupi ishirini ambazo zinathibitisha kwamba uwanja huu wa fasihi ya Kiswahili umefikia ukomavu wa hali ya juu katika vipengele vyake vyote: kimaudhui (ambayo ni anuwai: mapenzi, unyumba, siasa, uchumi, ucheshi, uana, utamaduni, mazingira, ufisadi, utandawazi na taathira zake kimataifa, n.k.); kimtindo na ujumi (ambao umezikoleza utamu na ladha hadithi zenyewe, hasa katika mtindo mpya wa fantasia na mkengeuko wa ukweli kama tunavyoujua kila siku). Bila shaka, mna ukwasi wa lugha, unaokwepa Kiswahili cha darasani; hasa kwa wingi wa ufundi wake uliojaa misamiati, jazanda, sitiari na tamathali zote za semi kwa ujumla.